Print Shortlink

Utafiti TAMWA Waonyesha Vipigo Kwa Wanawake Vimekithiri




 Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya.


 Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya akionesha ripoti hiyo kwa wanahabari.


 Mhariri Mkuu wa mtandao wa Thehabari.com (katikati) akiwa na
waandishi wengine katika uzinduzi wa taarifa hiyo. Kulia ni Sam Maella
wa ITV na Sanga wa Sanga wa The Citizen (kushoto).


 Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa taarifa hiyo ya utafiti.


 Baadhi ya wanahabari wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya alipokuwa akizindua ripoti ya utafiti.

Na Joachim Mushi,
CHAMA cha Waandishi wa
Habari Wanawake (TAMWA), kimewataka viongozi wote ngazi ya wilaya kwa
kushirikiana na wabunge kukemea vitendo vya unyanyasaji wa vipigo kwa
wanawake nchini.


Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya alipokuwa akizindua na kutoa ufafanuzi
juu ya utafiti uliofanyika hivi karibuni mikoa mbalimbali nchini, ambao
umebaini ongezeko la vipigo kwa wanawake.


Alisema katika ripoti ya utafiti huo mbali na kuibua masuala anuai
ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia imeonesha kuwepo kwa idadi kubwa
ya vipigo kwa wanawake vinavyofanywa na wanaume jambo ambalo
linakwamisha juhudi za maendeleo ngazi ya familia.

Alisema idadi kubwa ya wanawake vijijini ni wazalishaji mali wazuri,
hivyo endapo suala la vipigo litafumbiwa macho na Serikali kupitia
viongozi wake juhudu za maendeleo katika jamii zitakwamishwa.

“Ukatili
wa vipigo ni tatizo kubwa…na wote tunajua mtu anayepata kipigo kira
mara hawezi kuwa mzalishaji mali mzuri, suala hili likifumbiwa macho
umasikini mkubwa utaendelea kuzigubika familia zetu, hasa maeneo ya
vijijini,” alisema Nkya katika ufafanuzi wake.

Aidha alisema katika utafiti huo uliofanywa kwa ushirikiano na
waandishi kutoka vyombo anuai vya habari Tanzania, ukiwemo Mtandao wa
Thehabari.com baadhi ya viongozi ngazi za Wilaya wameonekana kuwa
vikwanzo katika utoaji wa taarifa hasa katika Wilaya za Tarime, Mvomero
pamoja na Wilaya ya Kinondoni.

Ameongeza kuwa utafiti umebaini kuwepo kwa baadhi ya watendaji hasa
wa vijiji kutofanya kazi zao ofisini jambo ambalo limekuwa kero kwa
wananchi na kushindwa kutimiza wajibu wao. 

Utafiti huo wa
kihabari (journalistic survey) uliofanyika kuanzia mwezi Aprili 2012,
TAMWA ulifanyika katika katika mikoa 20 ikiwepo 15 ya Tanzania Bara na
mitano ya Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine uliangalia vitendo
vya ukatili nchini. Vitendo vilivyolengwa ni ubakaji, vipigo kwa
wanawake, kutelekeza wanawake na watoto, ukeketaji na kulazimisha watoto
wa kike kulazimishwa kukatisha masomo na kuolewa.

*Habari hii imeandaliwa na Kuletwa Hapa na mtandao wa www.thehabari.com

Leave a Reply

You must be logged in to post a comment.